Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

Hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano-MorogoroHali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano-Morogoro
Utapiamlo ni hali ya upungufu wa lishe au lishe iliyozidi. Tunapozungumzia upungufu hapa tunazungumzia udumavu ambao ni utapiamlo wa muda mrefu (chronic malnutrition), ukondefu ambao ni utapiamlo wa dharura (Acute Malnutriton) na uzito pungufu (Underweight) ambao huonekana kwa watoto wenye udumavu na ukondefu. Vile vile utapiamlo unaweza kuwa wa upungufu wa virutubishi muhimu vya vitamini na madini ambavyo pamoja na kwamba mahitaji yake ni kidogo lakini umuhimu wake ni mkubwa sana kwa afya na Ustawi wa binadamu. Upungufu wa vitamin na madini unajulikana pia kama utapiamlo uliojificha au (hidden hunger) kwa kuwa madhara yake hayaonekani mapema. Aina nyingine ya utapiamlo ni ule wa lishe iliyozidi ambayo inapelekea magonjwa sugu yasiyoambukizwa yatokanayo na chakula, kama kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na hata baadhi ya kansa.
Sababu ya kuwepo kwa utapiamlo zimegawanyika katika makundi matatu:
1.      Sababu za karibu (immediate causes)
                                 i.            Ulaji duni na
                               ii.            Magonjwa
2.      Sababu zilizojificha (undelying causes) hizi ni zile sababu zinazopelekea uwepo wa sababu za karibu ambazo ni:
                                 i.            Upungufu wa uhakika wa chakula katika kaya,
                               ii.            Upungufu katika matunzo ya makundi maalumu ya watu, na
                             iii.            Upungufu katika huduma za msingi za afya katika jamii
3.      Sababu za Msingi (Basic causes) hizi ni zile sababu zinazopelekea kuwepo kwa sababu wezeshi na sababu za karibu:
                                 i.            Elimu duni
                               ii.            Rasilimali
a.       Udhibiti wa rasilimali watu, uchumi na rasilimali za mashirika
b.      Mfumo wa siasa na itikadi, Mfumo wa uchumi, mila na desturi
Sekta mtambuka zinahusika na kuzuia utapiamlo ni sekta za kilimo na uhakika wa chakula, Afya na Ukimwi, Maji, mazingira na usafi, Elimu, Maendeleo ya mtoto, usalama katika Jamii, Mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, Mipango, Maendeleo ya Jamii na Jamii kwa ujumla

Jinsi ya kuzuia utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano:
Jambo hili linatakiwa kuanza hata kabla wanawake hawajawa wajawazito. Hivyo ni muhimu kusimamia hali ya lishe ya wanawake katika umri wa kuzaa ili watakapokuwa wajawazito wawezeshe kukuwa vyema kwa kiumbe kinachokuja. Siku 1000 ni za Msingi sana katika kuzuia utapiamlo kwa watoto. Siku 1000 zinajumuisha siku 270 za ujauzito, siku 730 za mtoto katika miaka miwili ya mwanzo. Udumavu unaotokea na kutorekebishwa katika siku 1000 za kwanza hautaweza kurekebishwa tena.
Kuzuia utapiamlo:
Afua zinazolenga kupunguza/kuzuia udumavu na utapiamlo ni zile zinazolenga siku 1000 ambazo ni kuanzia mama anapokuwa mjamzito hadi mtoto anapofikia umri wa miaka miwili.
i.               Kuboresha lishe ya Jamii yaani watoto wadogo na wachanga, vijana, wanawake na wanaume
ii. Mama kuhudhuria kliniki mara anapojihisi mjamzito
iii.           Mjamzito kupata dawa za kuongeza damu madini chuma na aside ya foliki
                             iii.            Mjamzito kupata dawa za kutibu malaria na minyoo
                             iv.            Mwenza na Mjamzito kupata ushauri wa lishe, kupumzika wakati wa ujauzito na maandalizi ya Uzazi
                               v.            Matibabu ya magonjwa wakati wa ujauzito
                             vi.             Mama mzazi kupata dawa za kuongeza damu na nyongeza ya vitamin A katika siku 42 baada ya Uzazi
                           vii.            Mama mzazi anashauriwa kupata Huduma za Uzazi wa mpango ili awe na muda wa kulea mtoto na familia
                         viii.            Mama mzazi anashauriwa lishe yake mwenyewe wakati wa ujauzito na anaponyonyesha
                             ix.            Mama anashauriwa kunyonyesha mtoto maziwa ya mama tuu mara anapozaliwa kwa muda wa miezi sita ya mwanzo
                               x.            Mtoto aanzishiwe vyakula vya nyongeza mara anapofikia umri wa miezi sita huku akiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi atakapofikia umri wa miaka miwili au zaidi
                             xi.            Mama kumpeleka mtoto kliniki kwa ajili ya Huduma za chanjo ili kuzuia magonjwa yanayozuilika kwa chanjo
                           xii.            Ushauri unatolewa wa njia za kupata chakula kutoka makundi mbalimbali kwa kulima mbogamboga na kufuga wanyama wadogo
                         xiii.            Ushauri wa usafi wa mazingira, vibuyu chirizi na matumizi ya vyoo bora na kanuni za usafi zinatakiwa kuzingatiwa ili kuzuia magonjwa yanayoweza kupelekea utapiamlo kwa kuwa wakati wa ugonjwa watoto hukosa hamu ya kula hivyo kupelekea kupungua uzito na wanapopungua uzito hali zao za kinga hupungua hivyo kupelekea watoto kupata magonjwa ya mara kwa mara na mwisho hufikia hali ya utapiamlo
                         xiv.            Mikakati ya kupunguza utapiamlo yanatakiwa kufanyika katika sekta mtambuka za kilimo na uhakika wa chakula, afya na UKIMWI, maji na usafi wa mazingira (WASH), Elimu, usalama katika Jamii (Social protection), mazingira na mabadiliko ya tabia nchi na katika Ngazi ya Jamii kwa ujumla
                           xv.            Afua nyingine za kupunguza utapiamlo ni pamoja na urutubishaji wa vyakula kama vile nafaka kama unga wa ngano na mahindi zinaongezwa madini ya zinki na madini chuma, vilevile asidi ya folik na vitamini B 12. Mafuta ya kula huongezwa vitamin A na chumvi huongewa madini joto.
                         xvi.            Watoto hupatiwa nyongeza ya vitamin A na dawa za kutibu minyoo kila mwezi wa sita na wa kumi na mbili; Huduma hii hutolewa sambamba na kupima hali ya lishe na kisha kupatiwa matibabu kwa wenye utapiamlo mkaliHali ya lishe kwa Mkoa Morogoro
Hali ya udumavu katika mkoa Morogoro umepungua kutoka asilimia 44.4 (TDHS, 2010), asilimia 36.9 (NNS, 2014) na kufikia asilimia 33.4 (TDHS, 2015-2016). Malengo ya kitaifa ni kufikia asilimia 28 ifikapo mwaka 2021.
Hali ya ukondefu (utapiamlo wa dharura) ilikuwa asilimia 5 (TDHS, 2010) na kuongezeka mpaka asilimia 6 (TDHS, 2015-2016) malengo ni kufikia asilimia chini ya 5 mwaka 2021.
Upungufu wa damu kwa wanawake katika umri wa kuzaa ilikuwa asilimia 45 (TDHS, 2010) na imeongezeka kufikia asilimia 47.5 (TDHS, 2015-2016), kiwango hiki kinatakiwa kufikia asilimia 33 ifikapo mwaka 2021.
Upungufu wa damu kwa watoto chini ya miaka mitano imeongezeka kutoka asilimia 59 (TDHS, 2010) hadi kufikia asilimia 65.7 kwa (TDHS, 2015-2016).
Utekelezaji wa afua za lishe Tanzania unafuata mpango mkakati mtambuka wa lishe wa Taifa wa mwaka 2016-2021unaolenga watoto, vijana wanawake na wanaume wa Tanzania wawe na lishe bora itakayopelekea maisha na afya bora ambayo yataongeza uzalishaji na kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa taifa hivyo kufikia Maendeleo endelevu.
Maeneo saba ya kipaumbele ya Mkakati mtambuka wa lishe wa Taifa (2016-2021) ni:
·         Kuinua lishe ya wanawake katika umri wa kuzaa, watoto wachanga na wadogo na vijana
·         Kuinua mikakati ya kuzuia na kutibu upungufu wa vitamin na madini
·         Kuinua mikakati ya matibabu jumuishi ya utapiamlo wa dharura (ukondefu)
·         Kuzuia na kutibu magonjwa sugu yasiyoambukiza yatokanayo na chakula
·         Kuinua mikakati jumuishi ya lishe katika sekta mtabuka ambazo ni kilimo na uhakika wa chakula, afya na UKIMWI, maji na usafi wa mazingira (WASH), Elimu, usalama katika Jamii (Social protection), mazingira na mabadiliko ya tabia nchi
·         Kuimarisha mikakati ya lishe na utawala katika sekta mtambuka
·         Kuanzisha Uratibu wa takwimu za masuala ya lishe katika sekta mtambuka

Je lishe ni nini?
Lishe ni mchakato unaohusika tangu chakula kinapoliwa, kumengenywa na kuchukuliwa na seli za mwili kwa ajili ya matumizi katika mwili.
Makundi ya vyakula ambavyo vinashauriwa:
  1. Nafaka mizizi na ndizi mbichi
  2. Jamii ya mikunde na vyakula vitokanavyo na wanyama
  3. Mboga mboga
  4. Matunda
  5. Mafuta na sukari kwa kiasi
Bila kusahau maji ya kunywa safi na salama.

Post a Comment

0 Comments