Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

Dkt. Faustine Ndugulile Ameyataka Mabaraza ya Watoto nchini kutumia elimu wanayoipata kuibua vitendo vya ukatili.
  Mabaraza ya Watoto nchini yamehimizwa kutumia elimu wanayoipata kuibua vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto ili kuondokana na vitendo hivyo. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Watoto la Mkoa wa Mwanza alipowatembelea na kuona shughuli wanazofanya wajumbe wa Baraza hilo.
   Dkt.Ndugulile amesema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017 takribani wanawake na watoto 41,000 walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kati yao 13,000 wakiwa ni watoto pekee. Ameongeza kuwa vitendo vya ukatili vimeongezeka ukilinganisha na matukio ya vitendo vya ujambazi nchini ambapo suala hilo halitakiwi kufumbiwa macho na wananchi na wadau.
  Aidha Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa wananchi hasa wazazi na watoto kutomalizana nyumbani endapo vitatokea vitendo vya ukatili katika familia zao bali kuviripoti katika mamlaka husika. Naye Mwenyekiti wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Joel Festo ameishukuru Serikali na wadau kawa kuendelea kuwajali watoto kuanzia katika utoaji wa huduma za afya na kutekeleza upatikanaji wa haki zao za msingi ikiwemo haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushirikishwa na kutobaguliwa.
   Dkt Ndugulile pia ametembelea na kujionea shughuli zinazotolewa na Kituo cha utoaji Huduma za pamoja kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia (One Stop Centre) hapo mkoani Mwanza. Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure Dkt. Bahati Peter Msaki amesema kuwa Kituo cha utoaji Huduma kwa wahanga wa ukatili (One Stop Centre) kimekuwa msaada mkubwa kwa wanajamii kwani wahanga wengi wa vitendo vya ukatili wamekuwa wakipata huduma kutoka katika kituo hicho.

Post a Comment

0 Comments