Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

Mahakama Mkoani Njombe imeahidi kuweka mikakati ya kupunguza kesi za Watoto.
Mahakama ya hakimu mkazi mkoani Njombe imeweka mikakati ya kupunguza kesi za ubakaji, ulawiti na ukatili kwa kusikiliza mashauri ya watoto ili kudhibiti njia za rushwa miongoni mwa wazazi na watuhumiwa.

Hakimu Mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe  HASSAN MAKUBE amesema tabia ya baadhi ya wazazi kuweka vikao vya kumaliza kesi za ubakaji nyumbani imesababisha mahakama kushindwa kuwatia hatiani watuhumiwa.

Amesema  hali hiyo inasababisha  mashahidi wa kesi za ubakaji na ulawiti Kushindwa kuhudhulia mahakamani kutoa ushahidi na kuchangia watuhumiwa  kuachiwa huru pasipo haki ya mtoto kupatikana.

MAKUBE  amesema  Matukio ya ubakaji na ulawiti asilimia kubwa yanafanywa na  wanandugu  ambao wamekuwa na vikao vya kumaliza kesi hizo nyumbani na watuhumiwa kutoa fedha kinyume na sheria ili mashahidi wasifike mahakamani.

Kaimu mkuu wa Takukuru Mkoa  wa Njombe ALFEO LUNGWE amekili kuwepo changamoto ya wazazi kushiriki vikao vya kumaliza kesi za ukatili kwa watoto nyumbani na kupokea fedha kwa watuhumiwa huku akikemea vikali tabia hiyo ambayo inakwamisha maendeleo ya utoaji hukumu za kesi mahakamani.

Nae Mtendaji Wa Mahakama Mkoa Wa Njombe YUSUPH MSAWANGA akizungumza na kituo hiki, amesema ili kudhibiti na kutoa haki za watoto mahakamani, jamii inapaswa kukemea tabia za wanandugu kuendekeza vikao vya kumalizia nyumbani kesi za ubakaji wa watoto badala yake waiachie mahakama itende haki huku akiomba kuongezwa mahakama vijijini.

Kwa upande wa wananchi mkoani Njombe wamesema  vitendo vya ubakaji kwa watoto vinafanywa  na  wanandugu pamoja na baadhi ya akina baba  wenye imani potofu za kishirikina zinazowataka kubaka watoto ili kupata utajiri  huku wakitaka vyombo vya sheria kutunza siri za watoa taarifa za ukatili.

Na Michael Ngilangwa-Njombe.

Post a Comment

0 Comments