Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

MWALIMU JELA MIAKA 3 NJOMBE, KWA KUMSABABISHIA MWANAFUNZI ULEMAVU WA UTI MGONGO.


Mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe imemuhukumu mwalimu Focus Mbilinyi kwenda jela miaka mitatu kwa kosa la kumuadhibu na kumsabishia ulemavu wa uti wa mgongo   Hosea Manga  aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Madeke,Aidha mahakama imemtaka Focus Mbilinyi kulipa  shilling million 10 ikiwa ni  fidia ya gharama za matibabu alizozitumia mtoto hosea Manga Wa shule ya msingi Madeke iliyopo Wilayani  Njombe.

Akisoma hukumu hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Njombe Ivan Msaki amesema Mahakama imemuhukumu mwalimu Focus Mbilinyi kwa kosa la kujeruhi  kinyume na  sheria namba  225  kifungu kidogo cha 1 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 baada ya  kupitia  hoja za mashahidi watano wa upande wa jamuhuri na watatu wa upande wa utetezi ,Mahakama imejikita kwenye sheria ya elimu ya  utolewaji wa adhabu kama ulifuata utaratibu ukiwemo wa kusimamiwa na mkuu wa shule wakati adhabu inatolewa ambaye angethibitisha idadi ya viboko vilivyotolewa.

Hakimu Ivan Msaki  amesema ushaidi uliotolewa na shahidi wa kwanza ambae ni  Hosea Manga uliieleza mahakama kuwa alichapwa viboko kumi baada ya kukosa hesabu kumi huku akiwa amening’inizwa miguu juu kichwa chini ushahidi uliojumlishwa na shahidi mwingine  mwanafunzi Given Nyangwine na kuithibitishia mahakama kuwa mshtakiwa ametenda kosa.

Mahakama imeeleza ushahidi na kielelezo kilichotolewa kutoka taasisi ya mifupa Muhimbili idara ya upasuaji  uliotolewa na Daktari Silvery Mwesige aliyeieleza mahakama kuwa Hosea aliumizwa sehemu ya uti wa mgongo na kusababisha tatizo kwenye pingiri za  mgongo jambo lililopelekea damu kushindwa kufika sehemu ya chini ya mwili wake.

Hakimu Ivan amesema pamoja na upande wa utetezi  uliokuwa na mawakili Innocent Kibadu pamoja na Octavian Mbugani kuleta mkanganyiko wa ushahidi wa kukataa baadhi ya hoja, mahakama imeona mkanganyiko huo hauna maana kwenye kesi ya hiyo.
 
Katika kesi hiyo namba 141 ya mwaka 2019  Wakili wa serikali Radhia Njovu ameiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho na pia kumtaka mshtakiwa kulipa fidia kulingana na sheria ya fidia namba 348  kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20  kwa kuwa muathirika ametumia gharama kubwa za matibabu kuanzia alipoanza kutibiwa mpaka hivi sasa.

Mahakama imetoa siku 30 kwa mshtakiwa kukata rufaa katika Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa mwezi novemba mwaka jana . Mnamo tarehe 21  mwezi  machi mwaka 2017 Mtoto Hosea Manga mwenye umri wa miaka 12  akiwa darasa la tatu   katika shule ya msingi madeke anadaiwa kuadhibiwa na mwalimu huyo na kusababishiwa maumivu.Maumivu hayo yaliwafanya wazazi wake wachukua hatua za kumfikisha kwenye zahanati ya kijijini hapo na kisha  kuhamishiwa kituo cha afya  na baadaye kwenda hospitali ya misheni ya ikonda  kabla ya kufikishwa hospitali  ya kibena iliyokuwa hospitali teule ya mkoa wa njombe kwa wakati ule.

Hata hivyo Hosea alipewa rufaa na kuhamishiwa Dar es salaamu katika taasisi ya mifupa Muhibili  ambako aligundulika amevunjika uti wa mgongo na hivyo kupewa matibabu na kiti cha kutembelea huku akiendelea na matibabu.

 Baadaye kesi namba 83 ya mwaka 2017 ikafunguliwa dhidi ya mwalimu huyo nakisha  ikafutwa kutokana na daktari aliyemtibu kutoka hospitali ya muhimbili kushindwa  kufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa mara nane kabla ya kufunguliwa tena kwa mara ya pili novemba  2019 ambayo tamati yake imefikia  na kuamuliwa kwenda jela kutumikia mitatu.

    Na,Michael Ngilangwa-Njombe.


Post a Comment

0 Comments