Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

Chanzo cha wiki ya unyonyeshaji 1990 hadi leo.

WIKI YA UNYONYESHAJI DUNIANI 2020:
Afisa lishe mkoa wa Morogoro Bi, Salome Magembe ameelezea kuhusu chimbuko na uanzishwaji wa wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama,lengo likiwa kuielimisha jamii kuhusu wiki hiyo na kuona umuhimu wanawake kuwanyonyesha watoto wao tangu kujifungua hadi mtoto atakapo fikisha miaka miwili.

Kabla na baada ya miaka ya 1980 dunia ilishuhudia  tatizo la vifo vingi vya watoto wachanga na wadogo,Pamoja na juhudi za kuboresha huduma za afya, chanjo na matibabu ya magonjwa ya watoto bado hali ilibaki au kuzidi kuwa mbaya na tafiti mbalimbali zilifanyika ili kubaini visababishi vya vifo vya watoto. 

Baada ya tafiti hizo zilibaini uhusiano kati ya matumizi ya maziwa mbadala na vifo vya watoto hutokana na:

-Maziwa mbadala hayana viini vya kingamwili vilivyomo kwenye maziwa ya mama (Mfano Immunoglobin A) hivyo Watoto wasionyonya wanashambuliwa na maradhi kwa urahisi.

-Matumizi yasiyo salama ya maziwa mbadala kutokana elimu na duni ya walezi; maji yasiyo salama; uchafu wa vyombo; udhibiti duni wa bidhaa za maziwa mbadala; matumizi ya chupa za kulishia Watoto n.k. 

Aidha tafiti zilibaini kuwepo kwa ushawishi wa wasindikaji wa maziwa mbadala kwa wanawake ili waache kunyonyesha Watoto na badala yake watumie maziwa mbadala.
-Mbinu za ushawishi zilikuwa ni Pamoja na matumizi ya vyombo vya Habari, wafanyakazi wa vituo vya kutolea huduma za afya wakiwemo wauguzi, wakunga na madaktari.

-Promosheni katika jamii ambapo mawakala wa makampuni ya maziwa walifanya kampeni za uhamasishaji kwa wananchi.

-Utoaji wa maziwa ya bure, maziwa ya msaada unaokoma ili baadaye wazazi waanze kununua, ufadhili wenye malengo ya kuimarisha biashara na kadhalika.

Hata hivyo tafiti zilivumbua mambo mengi ikiwemo:-

Wanawake wanaofanya kazi za ajira wanashindwa kunyonyesha Watoto wao ipasavyo kwa sababu ya kukosa likizo ya uzazi ya kutosheleza kutimiza wajibu wao wa uzazi na jukumu lao la kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato na kukabiliana na changamoto za usawa wa kijinsia katika ajira na utumishi.

Iwapo Watoto watanyonyeshwa ipasavyo maziwa ya mama vifo vitapungua kwa kiwango cha asilimia 13 ambayo ni kiwango kikubwa kuliko afua zote za kupunguza vifo vya Watoto.

UNYONYESHAJI WATOTO MAZIWA YA MAMA ILIONEKANA KUWA NI AFUA INAYOONGOZA KATIKA KUPUNGUZA VIFO VYA WATOTO DUNIANI.

Mnamo mwaka 1990, mkutano wa wataalamu ulifanyika huko Innocenti katika mji wa Florence nchini Italia ili kujadili changamoto hizi na kutoa mwelekeo wa kisera kuhusu suala la kulinda, kuhimiza na kuendeleza unyonyeshaji Watoto maziwa ya mama kama njia kuu ya kulinda uhai na maendeleo ya Watoto.

Mkutano huo uliohisaniwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya WHO na UNICEF Ulifanyika tarehe 30 Julai na Tarehe 1 Agosti mwaka 1990,Wajumbe wa Mkutano waliafiki na kutoa azimio la Inocenti lililozitaka nchi wanachama kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kuweza kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo baada ya kujifungua, na kuendelea kuwanyonyesha watoto wao hadi watimize umri wa miaka miwili au zaidi. 

Wajumbe waliofikia Maafikiano hayo walikuwa ni wawakilishi wa nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Mashirika ya Umoja wa Mataifa hususan WHO na UNICEF,  na wadau wengine wa maendeleo,Wajumbe waliridhia na kusaini hati ya kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji maziwa ya mama kama njia pekee yenye ubora zaidi ya ulishaji watoto.  
Pamoja na mambo mengine Azimio la Inocenti liliagiza nchi wanachama,Kulinda, Kuhimiza na Kuendeleza  unyonyesha watoto maziwa ya mama,Kutunga na kutekeleza sharia na kanuni za kudhibiti uuzaji na usambazaji holela wa maziwa mbadala na vyakula vya Watoto wachanga na wadogo ili kulinda uhai na maendeleo yao.

Zahanati, vituo vya afya,hospitali na taasisi zinazotoa huduma za tiba na ukunga zitoe huduma Rafiki za kulinda unyonyeshaji,Wafanyakazi wa sekta ya afya wasitumike kuhamasisha matumizi ya maziwa mbadala na vyakula vya Watoto.

Kutunga na kutekeleza sharia za ajira na kazi zinazolinda haki ya uzazi ikiwemo haki ya wanawake wafanyakazi kunyonyesha Watoto bila kuathiri haki zao za ajira na kipato.

Aidha iliazimiwa kuanzisha maadhimisho endelevu ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani inayoadhimishwa ulimwenguni kote kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 7 Agosti . 

Wiki hii ya hamasa inalenga kuikumbusha jamii umuhimu wa unyonyeshaji watoto maziwa ya mama katika kujenga msingi imara wa afya na uhai wa watoto ambao ni taifa la kesho. 

Tangu kipindi hicho, Dunia imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani. 

Kupitia maadhimisho haya jamii inapata jukwaa la kukumbushana kuhusu umuhimu wa maziwa ya mama na jinsi yanavyosaidia kuboresha afya ya watoto wachanga, kuimarisha kinga mwili na ukuaji kimwili na kiakili.

Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani kwa mwaka 2020 yamebebwa na kauli mbiu inayosema “Tuwawezeshe wanawake kunyonyesha kwa afya bora na ulinzi wa mazingira”. 

Yafuatayo ni Malengo ya Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama kwa mwaka 2020: 

Kuhamasisha jamii iendeleze juhudi za Kulinda, Kuhimiza na Kuendeleza unyonyeshaji watoto maziwa ya mama kama njia mojawapo ya kutunza mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. 

Kuimarisha fikra za jamii kwamba Kulinda, Kuhimiza na Kuendeleza unyonyeshaji watoto maziwa ya mama ni mojawapo ya maamuzi sahihi ya kutunza mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. 

Kuishirikisha jamii katika juhudi za Kulinda, Kuhimiza na Kuendeleza unyonyeshaji watoto maziwa ya mama ili kupata matokeo chanya. 

Kushawishi ushiriki wa jamii katika mikakati ya kuboresha afya kupitia Kulinda, Kuhimiza na Kuendeleza unyonyeshaji.

Post a Comment

1 Comments

  1. If your looking for Online Illinois license plate sticker renewals then you have need to come to the right place.We offer the fastest Illinois license plate sticker renewals in the state. jobber wiki

    ReplyDelete