Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

Watoto wanaelewa nini kuhusu mabaraza yao?


Na. John Kabambala, TKT/UN RADIO.

Katikati ya Manispaa ya Morogoro, ipo shule ya msingi iitwayo Mwere. Shule ya Msingi Mwere inapakana kabisa na Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za mkoa wa Morogoro. Shule hii ipo takriban meta 200 kutoka zilipo ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Asubuhi moja, kama saa nne na nusu hivi, napita shuleni hapo. Ni muda wa mapumziko. Wanafunzi wako nje wakicheza michezo tofauti katika viwanja vya shule yao. 

Naingia katika kundi mojawapo la watoto. Wanaponiona, wanasita kuedelea namichezo yao. Mmojawao ananiamkia nawengine wanafuatia kila mmoja kwa wakati wake. Kwa pamoja nawaitikia, marahaba watoto wazuri hamjambo? Nao kwa pamoja wanaitika “hatujambo”.

Baada ya maamkuzi hayo, Napata fursa ya kuwauliza maswali ya ufahamu kuhusu masuala tofauti. Lengo langu hasa nikufahamu iwapo wana uelewa kuhusu masuala kadha wa kadha yanayo wagusa.

Swali langu lilikuwa dogo tu, nalo lilihusu iwapo watoto hawa wana fahamu au wamewahi kusikia kuhusu baraza au mabaraza ya watoto?

Watoto waliopata nafasi ya kuzungumza nami kupitia TKT/UNRADIO walionekana kutofahamu mabaraza hayo. Binti aliyejitambulisha kwa jina la Sabrina Hamisi Dimoso alisema hayafahamu mabaraza hayo. 

Mwingine ni Abubakari Shabani alisema: “Mabaraza hayo yangetusaidia kutoa kero na maoni yetu, kwani na sisi tuna mambo ambayo tunaogopa kuwambia  watu wazima. Lakini kama mabaraza haya yakiwepo watoto wengi wangezungumza na viongozi wetu kwa sababu tuna umri unaoendana, hatuogopani” Pia mtoto Abdulazizi Mfaume kama wenzake alisema hajawahi kusikia kuhusu mabaraza ya watoto.

Majawabu tofauti yalitoka nje ya shule ya Mwere ambakoTKT/UNRadio ilikutana na mtoto Asia Makame (17), ambaye ni mjumbe wa Baraza la Watoto ngazi ya taifa. Yeye alisema mabaraza ya watoto yaliundwa, isipokuwa hayafanyi kazi katika baadhi ya maeneo. 

Asia alisema changamoto iliyopo ni mitazamo tofauti miongoni mwa wazazi na walezi, kuhusu watoto wao kujiunga na mabaraza hayo. Alisema wanayahusisha na masuala ya vyama vya siasa.“Jambo hili siyo kweli, kwani huwanyima fursa watoto ya kujumuika na kushirikiana na watoto wenzao,”alisema Asia.

Majawabu ya watoto na uelewa wao kuhusu mabaraza yao, yalitusukuma kutafuta ukweli kuhusu historia na utendaji wa mabaraza ya watoto kutoka kwa wadau mbali mbali wakiwamo viongozi wa kijamii katika ngazi za chini.

Miongoni mwa viongozi hao ni Shimba Mayunga ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigurunyembe katika Manispaa ya Morogoro. Yeye alipoulizwa kuhusu uelewa wake katika suala la mabaraza ya watoto alisema: “Sija wahi kusikia mabaraza ya watoto. Kuna kero ndogo ndogo zinazowahusu watoto wenyewe, hivyo lazima wawe na baraza lao ili wapate pahali pa kuzungumzia”.


Baraza la Watoto

Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilianzishwa Mei,2002, chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. 

Lengo la kuanzishwa kwa baraza hili ni kutekeleza haja ya moja ya haki za watoto ya kupewa nafasi ya kushiriki. Haki hii huwawezesha watoto kutoa maoni yao ili yaweze kuzingatiwa katika kuandaa na kutunga sera na sheria mbalimbali zinazogusa haki na ustawi wao, katika ngazi zote kuanzia mtaa/kijiji, kata, wilaya namkoa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akizungumzia mabaraza ya watoto alisema Sheria ya mtoto ya Tanzania ya 2009 haizungumzii moja kwa moja kuhusu uanzishwaji wa mabaraza ya watoto.

Hata hivyo Henga alisema Sheria hiyo imetoa mwanya wa kanuni ya ulinzi wa mtoto kupitia mpango mkakati wakupinga ukatili wa wanawake na watoto, hivyo basi baraza la watoto ni utekelezaji wa sheria zilizomo kwenye mikataba ya kimataifa na kikanda.

Kauli ya Serikali

Mkurugenzi wa Watoto, kutoka Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ya Wizara ya Afya, Bibi Mwajuma Magwiza alisema kuna idadi kubwa ya mabaraza ya watoto yaliyoundwa kuazia ngazi za mitaa na vijiji, kata, halmashauri, wilaya, mikoa na ngazi ya taifa.

“Katika ngazi za mitaa na vijiji tuna mabaraza765, ngazi ya Kata ni mabaraza733, ngazi ya Halmashauri ni mabaraza 121 kati ya halmashauri 184 nchi nzima, katika ngazi ya mkoa kuna mabaraza 19 na ngazi ya taifa kuna baraza 1. Kwa ujumla nchi nzima kuna mabaraza 1,696,” alisema mkurugenzi huyo.

Kuhusu malengo yaliyo kusudiwa Bibi Mwajuma alisema yametimia. “Lengo limetimia kwasababu lengo lilikuwa nikutoa fursa ya watoto kushiriki katika kutoa mawazo,michango yao hususani maendeleo yanayo wahusu wao, pia kuanzisha mabaraza haya ngazi zote ilikumuwezesha mtoto katika kila ngazi kushiriki kuanzia, vijiji/mtaa, kata, wilaya, mkoa nangazi ya Taifa”.

Kauli ya Bibi Magwiza inajiakisi mkoani Morogoro, ambakoTumaini Wapalila ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa mkoa huo, alisema tangu mwaka 2009 walianza kuunda mabaraza ya watoto kwa ngazi zote kwa mujibu wa mwongozo wa uundwaji wa mabaraza ya watoto.

Alisema hadi sasa kwa mkoa wa Morogoro mabaraza yanayofanya kazi ni katika halmashauri tatu ambazo ni Manispaa ya Morogoro,Wilaya ya Mlimba na Mamlaka ya Mji mdogo wa Ifakara.

Serikali hushirikiana na wadau wengine utekelezaji wa shughuli za kijamii. Katika utekelezaji wa shughuli za mabaraza ya watoto, yapo mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali ambayo yamekuwa ya kitoa mchango wake. Miongoni mwa mashirika hayo ni Plan International ambalo limekuwa likifanya kazi zake mkoani Morogoro. 

Mmoja wa watendaji wa taasisi hiyo, Simoni Mabagala alisema Plan International wameshiriki kwa kiasi kikubwa kuyauhisha mabaraza ya watoto katika ngazi mbalimbali kuanzia mitaa/kijiji, kata na mamlaka za miji na wilaya.

Alisema taasisi yake imekuwa ikiyaunga mkono mabaraza hayo kwa kutoa misaada ya kifedha kila kunapokuwa na uhitaji wa kufanya shughuli husika. Shughuli hizo zinajumuisha uendeshaji wa vikao vya kila robo mwaka, maadhimisho ya kila mwaka yanayowahusu watoto na kuweka mfumo wa kusimamia fedha hizo, ili kuhakikisha malengo yanayokusudiwa yanatimia.


Mwisho…

Post a Comment

0 Comments