Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

ATHARI ZA NDOA ZA UTOTONI KIAFYA

Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 haiwalindi wasichana dhidi ya kuolewa, Sheria hii imekuwa ikipigiwa kelele ifanyiwe marekebisho kwa mda mrefu ingawa hadi sasa hakuna majibu sahihi kutoka kwa mamlaka husika. Sheria hii inaruhusu wasichana wenye miaka 14 kuolewa kwa (ruhusa maalum ya wazazi), inaruhusu wasichana wenye umri kuanzia miaka 15 kuolewa iwapo umbile lao linaonekana kubwa, Hali hii ina athari kwa maendeleo ya mtoto na Taifa kwa ujumla wake.


TATIZO LA NDOA ZA UMRI MDOGO
Ndoa za umri mdogo ni suala la afya pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, kwani wasichana walioolewa kwa umri mdogo wana uwezekano mkubwa wa kupata madhara ya kiafya ambayo yaweza kudumu katika miili yao au kupelekea vifo.

Ndoa za utotoni ndio sababu kuu ya kupata watoto katika umri
Mdogo, Makadirio ya Benki ya Dunia yanadokeza kwamba watoto wawili 2 kati ya watatu 3 (65%) waliozaliwa na mama mwenye umri chini ya miaka 18 walitokana na ndoa za utotoni, na kwamba idadi sawa na hiyo (65%) ya wanawake waliopata watoto kabla ya umri wa miaka 18 ilikuwa ni matokeo ya ndoa za utotoni.

CHANZO CHA TATIZO HILI NI NINI?
Mbali na ukinzano wa Sheria ya Ndoa na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, umaskini, Ukosefu wa elimu, Kuchukuliwa hali ya chini ya wasichana na ubaguzi wa kijinsia ni mojawapo ya sababu zinazo changia kuendelea kwa vitendo hivi vya kuozesha watoto katika umri mdogo.

Ndoa za umri mdogo ni aina ya ubaguzi wa kijinsia ambao unawagusa wasichana wadogo, na kuwafanya waendelee kua waathirika wa kuambukizwa magonjwa mbali mbali kwa urahisi wakilinganishwa na wenzao ambao hawajaolewa, na hakuna uwezekano wa wasichana hao walioolewa kupanga uzazi.

Nimefanya mahojiano na Daktari bingwa wa magonjwa ya akina Mama, Dkt.Nyasinde Mujumali yeye amezitaja baadhi ya athari anazo wezakuzipata mtoto wakike atakapo olewa katika umri mdogo.

ATHARI ZAKE KIAFYA:
Athari za ndoa za utotoni kiafya nikupata mimba kabla ya wakati, Hatari ya kukumbwa na matatizo katika ujauzito wakati wa kujifungua, Vifo vya akina mama na watoto wachanga, Utapiamlo, Wasiwasi na mafadhaiko (wasichana na wavulana) na Msongo wa mawazo.

Aidha Dkt. Nyasinde anasema madhara mengine anayoweza kuyapata mtoto anapokua mjamzito, inaweza kuwa vigumu sana kutambua hatua zote zinazo onyesha kwamba ni mjamzito, kutambua vyakula anavyo paswa kula kwafaida yake na lishe ya mtoto aliopo tumboni, shinikizo la damu wakati mwingine hupekea kifafa cha mimba, upungufu wa damu, fistula, maambukizi ya magonjwa ya zinaa yanayo weza kusababisha madhara kwake na mtoto wake.

“Tatizo la afya ya akili kwa sasa linawakumba pia vijana walio katika umri mdogo, na linaweza kuzidi kwa mtoto huyu alie ingia kwenye ndoa akiwa katika umri mdogo kwa kuwa na msongo wa mawazo muda mwingi, inawezekana ameingia kwenye ndoa kwa kulazimishwa na wazazi bila ridhaa yake, au kwa sababu ya kupata msaada wa kifedha kutoka kwa muoaji ili familia yake isadiwe, hivyo machungu anayo kutana nayo kwenye ndoa ni magumu kuzidi uwezo na umri wake”. Dkt.Nyasinde amesema.

Katika Manispaa ya Morogoro nimekutana na Jarimo Joakim sio majina yake halisi, huyu ni miongoni mwa wahanga wa ndoa za utotoni nchini Tanzania, aliolewa akiwa na umri wa miaka 17 tu wakatihuo akiishi kijiji cha Dumila Wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro.

Alibeba ujauzito na alipojifungua baada ya siku nne (4) alipata kifafa cha mimba, akarejeshwa hospital kwa ajili ya kupata matibabu Zaidi, Jarimo Joakim anasema chanzo cha kuingia kwenye ndoa ni ugumu wa maisha, mama yao kuikimbia familia na kuwaacha wadogo wakilelewa na baba yao pekee, wakati mwingi waliishi peke yao wakati mzazi wao huyo mmoja akiwa kwenye utafutaji.

Chapisho lililo andaliwa na taasisi ya Msichana Initiative na Twaweza Nisisi kuhusu ndoa za utotoni linaonesha wastani, wanawake ambao waliolewa utotoni wana watoto watatu, na walipata mtoto wa kwanza wakiwa na umri wa miaka 17, wakati wanawake waliolewa katika umri mkubwa wana watoto watatu, walianza kupata mtoto wa kwanza katika umri wa miaka 22. Na 58% ya wanawake waliolewa utotoni walipata watoto kabla ya kutimiza umri wa miaka 18 ikilinganishwa na 10% ya wanawake walio olewa wakiwa na umri wa miaka 20 au zaidi.

Joakim ni mkaazi wa Dumila Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro ndie baba yake Jarimo Joakim, anasema alivyo pata taarifa ya kwamba mtoto wake ametoroshwa na mwanamume alianza kufuatilia na kufanya uchunguzi na kubaini kuwa mwanae amekwisha pata ujauzito. Kijana aliekuwa amemtorosha alipo sikia kwamba anatafutwa kukamatwa, akatoroka kusikojulikana kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.

Ndugu Joakim anamtupia lawama mzazi mwenzake alie toroka nyumbani hapo kwenda kuolewa na mume mwingine na kuwaacha watoto wao wakiwa bado wadogo, “anasema jambo hilo ndilo lililosababisha nguvu ya malezi na uangalizi ikapungua kwani muda mwingi na mimi ninakuwa kwenye mihangaiko ya kutafuta mahitaji ya msingi kwa ajili yao. Hivyo watoto hubaki wenyewe kuanzia asubuhi hadi jioni na wakati mwingine naweza kukaa nje ya nyumbani kwa Zaidi ya siku tano”.

Herriet Mkaanga yeye ni mchechemzi wa masuala ya watoto wakike na wasichana walio katika umri wa kuolewa, anasema hukutana na watoto wakike mara kwa mara walio katika umri mdogo wakiwa na watoto wao, anapo zungumza nao hubaini asilimia kubwa wameolewa katika umri mdogo. “Undani wake Zaidi unakuta chanzo cha kuolewa katika umri huo ni ugumu wa maisha, ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi kwa wazazi na kwa mtoto wakike mwenyewe”.

KWA NINI MILA HII HUTEKELEZWA?
Mbali na ukinzano wa Sheria ya Ndoa na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Ukosefu wa kipato cha kutosha kwenye familia, Ukosefu wa elimu, Kutengana kwa wazazi na kuchukuliwa hali ya chini ya wasichana na ubaguzi wa kijinsia ni mojawapo ya sababu zinazo changia kuendelea kwa vitendo hivi vya kuozesha watoto katika umri mdogo.

UTATUZI WA TATIZO HILI NI NINI?
Dr. Nyasinde anasema jamii inapaswa kuelewa kwamba mtoto wakike anapo ozeshwa katika umri mdogo nisawa na kumuandalia fungu la matatizo maishani mwake, na suluhisho lake nikuwapa nafasi ya kuwa watoto, kumaliza masomo yao kwa maendwleo yao,
familia na jamii.

Ndugu Joakim yeye ambae ameyaonja machungu dhidi ya mtoto wake kuolewa katika umri mdogo anaiomba Serikali itilie mkazo wa Sheria ya mtoto, pamoja na jamii kushirikiana pasipo kufimbia macho, wale wanao warubuni watoto wakike wakamatwe ilikkukomesha tabia hii chafu.

Kwa upande wake bi, Herriet Mkaanga anashauri ilikukomesha vitendo hivi vya kuozesha watoto wadogo ni lazima vifanyiwe maboresho vifungu vya Sheria ya ndoa pamoja nakuweka mkazo Zaidi namna ya utoaji adhabu kwa mtuhumiwa wa aina hii.

Jicho la mwandishi wa Makala hii: Jamii ya watanzania wanaoishi ndani nanje ya Tanzania, nimuda sasa wa kuungana na wadau wa maendeleo nchini kuhusu Serikali kufanya maboresho ya vifungu vya Sheria ya ndoa ya mwaka 1971, vinavyo ruhusu mtoto wakike kuolewa.
Na, John Kabambala.

Post a Comment

0 Comments