Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

UMUHIMU WA LISHE SHULENI MOROGORO.

 

Na, John Kabambala - Morogoro. 
Kuboresha lishe ni msingi katika kufanikisha malengo yote ya Kitaifa na Kimataifa hasa kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Maitaifa (SDGs). Uwepo wa utapiamlo sugu yaani  (udumavu) unadhoofisha maendeleo katika uhakika wa chakula, uboreshaji wa elimu, na afya bora ya mama na mtoto nchini.

Lishe duni ndio sababu kubwa ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano nchini Tanzania na inakadiriwa kugharimu serikali asilimia 2.6 ya Pato la Taifa kila mwaka. Upotezaji huu wa mapato uko katika sekta ya kilimo na husababishwa na ukuaji duni wa akili na mwili unaotokana na utapiamlo.

MWAKA 2015-2016 HALI YA LISHE ILIKUWAJE?

Kulingana na Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya ya mwaka 2015-2016, takriban theluthi ya watoto wote chini ya miaka mitano walikuwa na udumavu na asilimia 14 walikuwa na uzito upungufu, Sababu kuu zinazoongoza kuleta utapiamlo ni ukosefu wa lishe mchanganyiko na bora kwa kila kaya, upatikanaji mbovu wa huduma za afya (pamoja na maji safi na salama, usafi wa mazingira), na mienendo duni ya lishe.

WAKATI HUO MKOA WA MOROGORO HALI YA LISHE ILIKUWAJE?

Licha ya maendeleo na juhudi za serikali katika kuhamasisha kilimo chenye tija, utatuzi wa lishe duni kwa watoto bado nimekuwa changamoto kubwa,katika Mkoa wa Morogoro, chati ifuatayo inaonesha hali ya lishe ya Mkoa huo kuanzia 1992-2018.

Kama sehemu ya mkakati kamili wa lishe, USAID inazingatia kupunguza kiwango cha udumavu nchini Tanzania kupitia mipango na huduma za afya na kilimo katika ngazi za wilaya na jamii. Uwekezaji muhimu kwenye lishe ni pamoja na, kuimarisha Taasisi za Serikali za Tanzania na asasi za kijamii (AZAKI) zinazoshughulikia masuala ya lishe, kuongeza juhudi za mabadiliko ya kijamii na mienendo ili kuboresha namna ya ulishaji wa watoto wachanga na wadogo na kuongeza upatikanaji wa lishe yenye afya, lishe mbalimbali kwa mama na watoto.

Mradi wa lishe wa USAID uliambatana kabisa na Mpango wa Utekelezaji wa Lishe ya Kitaifa wa Tanzania (2016-2021), Mpango mkakati huo uliithibitishia Serikali ya Tanzania ahadi ya kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano (5) kutoka asilimia 34 hadi asilimia 28 ifikapo mwaka 2021.

UDUMAVU NI NINI?

Udumavu ni hali inayotokea wakati uwiano kati ya urefu na umri vinakuwa chini kwa vigezo vya ukuaji vilivyowekwa na shirika la afya duniani. kwa jina jingine udumavu unaweza kuelezewa kuwa ni udhaifu wa ukuaji wa mwili na maendeleo ya ukuaji wa mtoto unaotokea kwa mtoto kutokana na lishe duni, kuugua mara kwa mara na kukosa msisimuo wa kisaikolojia na kijamii.

UMUHIMU WA LISHE SHULENI

Umuhimu wa mpango huu ni kumwezesha kijana rika balehe kuelewa mbinu bora za kuhakikisha anapambana na udumavu katika familia yake na pia atakapokuwa mzazi baadae , kikubwa muhimu kijana rika balehe yupo kwenye kipindi ambacho anapevuka hivyo anahitaji vyakula vyenye mchanganyiko wa makundi yote Matano ili kuweza kumsaidia katika kipindi hiki muhimu.

SABABU ZA WATOTO KUDUMAA

Lishe duni na kuugua mara kwa mara katika kipindi cha siku 1000 za mwanzo za maisha ya mtoto, Taratibu duni za ulishaji watoto wachanga na wadogo, ikiwemo watoto kutonyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa, na kupewa chakula cha nyongeza kisichokidhi mahitaji yao kilishe pale wanapotimiza umri wa miezi sita, na hadi umri wa rika balehe.

 Afya na lishe duni ya wanawake kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua. Wanawake kuwa na kimo kifupi; kutopangilia uzazi na hivyo kuzaa karibu karibu; na tatizo la wasichana kupata mimba wakiwa katika umri mdogo.

MADHARA YA UDUMAVU:

Mtoto akidumaa hupata athari zisizoweza kurekebishwa kwani athari hizo hudumu katika maisha yake yote, Udumavu husababisha kupungua kwa kasi ya maendeleo ya ukuaji wa akili hali inayosababisha watoto kupata matokeo duni kielimu, Udumavu husababisha kupungua kwa kasi ya maendeleo ya ukuaji kimwili hali inayosababisha watoto kuwa na afya duni.

Kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi hali inayosababisha kupungua kwa tija na mapato kiuchumi, Kuongezeka kwa uwezekano wa watoto waliodumaa kuwa na uzito uliozidi au kiribatumbo, kuugua magonjwa ya moyo, kiharusi, shinikizo kubwa la damu, na kisukari wakati wanapofi kia umri wa utu uzima.


 MRADI WA USAID-LISHE ENDELEVU UMELIFANYA YAPI?

Kupitia mradi wa USAID/Lishe Endelevu uliokuwa ukitekelezwa nchini kwa mikoa minne ukiwemo Mkoa wa Morogoro chini ya Shirika la Save the Children kwa kushirikiana na Asasi za kiraia ikiwemo UMWEMA kwa Mkoa wa Morogoro, ili kuhakikisha wanayafikia malengo ya kupunguza Udumavu kwa Watoto na Vijana balehe ulianzisha mpango wa kuhamasisha afua za lishe kwa vijana balehe mashuleni ilikuwapa mbinu wezeshi vijana rika jinsi ya kuweka kipaumbele aina ya vyakula wanavyotakiwa kula.

Akizungumza kwa niaba ya meneja wa asasi ya Umwema Bi, Felista Mwalongo ameniambia kwamba,  malengo ya uhamasishaji afua za lishe, ulilenga kuwafundisha ratiba ya vyakula kuanzia asubuhi hadi usiku huku wakiwezeshwa kupata mbinu mbalimbali za kuhakikisha kuna upatikanaji wa chakula cha kutosha, kwa makundi yote 5 wawapo nyumbani kwa kuwasaidia wazazi wao namna ya upangaji milo na kuandaa bustani majumbani.

Pia kuanzisha bustani za mfano mashuleni ambazo zinatumika kuwapa ujuzi vijana ili waweze kwenda kuzifanya nyumbani na kuwa washauri wazuri juu ya masuala ya Lisha katika jamii inayomzunguka hasa kwa vijana rika balehe ambao hawakubahatika kupata mafunzo hayo.

MBINU ZIPI ZILITUMIKA KUTOA ELIMU HII?

Mbinu zilizo tumika ni michezo iliyokuwa nalengo la kumuandaa kijana kujua akitumia aina fulani ya chakula bila kujali yale makundi Matano nini athari yake, Pia jinsi ya kujua kuweka vipaumbele pindi anapotaka kufanya manunuzi ya aina yoyote baada kuuza mazao aliyoweza kuzalisha kupitia shughuli za shamba na ufugaji.

MRADI ULIFANIKIWA KWA KIASI GANI?

Mafanikio ya mpango huu ni kuweza kuwafikia vijana wa rika balehe mashuleni kwa asilimia mia kulingana na malengo ya mradi, hivyo kwa kiwango hicho cha vijana waliofikiwa wamekuewa chachu katika familia zao ambako huko kuna Watoto chini ya miaka miwili ambao wameweza kuondokana na udumavu kupitia vijana rika balehe kuhamasisha afua za lishe kwa wazazi wao.

Mpango huu umeweza kuwaongezea vijana rika balehe kufanya chaguzi sahihi ya vyakula walavyo kwani wamejua ni bora kula chakula chenye kukuletea virutubishi kuliko kupenda kula vyakula visivyo na faida katika mwili

Programu ya Lishe endelevu ilitumia utaratibu wa kuunda klabu za lishe ambapo huko ndiko vijana waliweza kupata elimu na mbinu mbalimbali,Vijana wa lika balehe baada ya kupata elimu shuleni kupitia club zao waliweza kwenda kuzifanya  majumbani kwao na jamii kwa ujumla, Mfano mzuri wa shule ambayo ilifanya vizuri wakati wa utekelezaji wa mpango huu ni shule ya sekondari Mafiga, Mbinu pekee zilizotumika katika shule hii ni uhamasishwaji ambao ulifanyika kupitia mwalimu aliyeteuliwa kusimamia clabu iliyoundwa shuleni.

Shule hii iliweza kuwa na bustani ya mbogamboga na matunda ambayo kila mwanaclabu alihamasika kuihudumia ili mwisho wa siku waweze kutumia vyakula vilivyopatikana katika eneo la shule yao, na hata kupitia bustani walizo zianzisha nyumbani kwao kwa kushirikiana na wazazi.

CHANGAMOTO WAKATI  WA UTEKELEZAJI.

Kuna changamoto chache ambazo ziliukabili mpango huu ikiwa nipamoja na Ukame na ukosefu wa maji kwa baadhi ya shule kupelekea bustani za mfano kukauka, kuhamahama kwa waalimu ambao walipewa mafunzo ya jinsi ya kutumia zana za kufundishia. Pia bustani zilihitaji vifaa vya kutunzia kama keni za kumwagilia hivyo sio shule zote ziliweza kuwa na vifaa vya umwagiliaji.

 NINI KIFANYIKE ILI KUZUIA UDUMAVU?

Tuhakikishe kuwa wanawake wanakuwa na hali nzuri ya lishe wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha baada ya kujifungua, pia vijana balehe wahamasishwe umuhimu wa lishe katika makuzi yao ilikuondoa udumavu kwenye familia zao.

 

 

Post a Comment

0 Comments