Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

KUTOKOMEZA UTUMIKISHWAJI WA WATOTO TANZANIA.

 


HALI YA UTUMIKISHWAJI IPOJE WILAYANI SONGWE?

Na, John Kabambala: Wilaya ya Songwe iko katika Mkoa wa Songwe nchini Tanzania. Ilianzishwa rasmi Mwezi September,2015 na ni moja kati ya Wilaya mpya zilizoanzishwa baada ya kugawanywa kwa Mkoa wa Mbeya.

Kuhusu utumikishwaji wa watoto katika kilimo cha zao la tumbaku Wilaya ya Songwe, ni jambo ambalo limekuwa likijitokeza katika maeneo mengi ya Tanzania, ikiwemo wilaya hiyo. Utumikishwaji wa watoto katika kilimo ni suala la kusikitisha ambalo linawanyima watoto haki zao za msingi, kama elimu na afya, na kuwaweka katika hatari ya kudhurika kimwili na kisaikolojia.

Tumbaku ni zao muhimu la biashara nchini Tanzania, na wilaya ya Songwe imekuwa moja ya maeneo yenye kilimo kikubwa cha zao hilo, kwa bahati mbaya, watoto wamekuwa wakitumikishwa katika hatua mbalimbali za uzalishaji wa tumbaku, ikiwa ni pamoja na kulima, kuvuna, kukausha na hata kusaidia katika usindikaji wa tumbaku.

CHANZO CHA TATIZO HILI?

Familia nyingi hapa kijijini shughuli za kiuchumi zinategemea kilimo cha tumbaku, zamani kabla ya kuletwa mradi wa kupinga utumikishwaji wa watoto Prosper mashambani walitumia watoto wao kama nguvu kazi, ndio maana kuna Shule Fulani kwenye kata hii kufelisha darasa zima ilikuwa kawaida tu. Maana wazazi wengi walishindwa kuthamini umuhimu wa elimu, ila kilimo cha zao la tumbaku wakakipa kipaumbele, Lakini sasa hali hiyo imepungua sana” Alisema Maria Kawana mkaazi wa kijiji cha Gua Kata ya Gua Wilani Songwe.

Tanzania ni miongoni mwa nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) zilizoridhia Mikataba yote inayolenga kuwalinda, kuwatetea na kuendeleza haki za Watoto. Mikataba hiyo ni Mkataba wa Haki za Mtoto wa 1989 wa Umoja wa Mataifa, Mkataba ya Shirika la Kazi Duniani Na. 138 unaohusu umri wa chini wa mtoto kuajiriwa na Na. 182 Unaohusu kazi hatarishi zisizoruhusiwa kufanywa na Mtoto.

Serikali imekuwa mstari wa mbele tangu mwaka 1994 kupambana na tatizo la utumikishwaji wa watoto kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kwa kuweka Mipango na Mikakati ya kitaifa na sheria zinazotekelezwa hapa nchini.

Sababu kuu za utumikishwaji wa watoto katika kilimo cha tumbaku ni umaskini, ukosefu wa elimu, na mazingira duni ya kijamii. Watoto wengi hulazimika kusaidia familia zao katika shughuli za kilimo ili kusaidia katika kupata kipato cha familia. Aidha, kukosekana kwa fursa za elimu na ufikiaji mdogo wa huduma za kijamii katika wilaya hiyo huwafanya watoto wawe katika hatari zaidi ya utumikishwaji.

Serikali ya Tanzania na mashirika ya kitaifa na kimataifa yamechukua hatua kadhaa za kukabiliana na tatizo hili, miongoni mwa mashirika ya kitaifa ni TDFT ambalo nimekuwa likitekeleza mradi wa Prosper Reset unao waondoa watoto wanaotumikishwa katika kilimo cha zao la Tumbaku kwa Mikoa mitatu Tanznaia ambayo ni Tabora, Mbeya na Songwe.

Ndg. Fredrick Malaso yeye ni meneja mradi wa Prosper Reset anasema tangu mwaka 2011 mradi huo ulianza kutekelezwa katika Wilaya tatu za mkoa wa Tabora (Sikonge,Urambo na Kaliua), kufikia mwaka 2018 mradi uliongeza Wilaya mbili Chunya na Songwe kutoka kwenye Mikoa ya Mbeya na Songwe.

                                    
                      MATOKEO YA MRADI HUO:
Ndg.Malaso amesema mojawapo ya mafanikio ya mradi huo ni pamoja na kuwaondoa watoto 24,150 kutoka katika utumikishwaji, na kusaidia kaya 970 kuwapa elimu ya kuanzisha shughuli za ujasiliamari na biashara ndogondogo za kuongeza kipato kupitia vikundi 56 vilivyo anzishwa na kusimamiwa na Mradi huo.

Kwa upande wake Afisa kazi Mkoa wa Songwe Bi, Pendo Lugendo amebainisha kwamba, Sheria za kazi zinakataza utumikishwaji wa watoto, na kuna juhudi za kuongeza uelewa kuhusu haki za watoto na kuzuia utumikishwaji kupitia elimu na mafunzo kwa wazazi na jamii kwa ujumla.

Pamoja na changamoto hizo, jitihada za Serikali na Wadau wanashirikiana kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki zao za msingi na wanakuwa katika mazingira salama na yenye maendeleo, ili kutokomeza utumikishwaji wa watoto katika kilimo cha tumbaku na maeneo mengine ya Wilaya ya Songwe.

JE, SULUHISHO NI NINI/NINI KIFANYIKE

Vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuongeza uelewa na kuhamasisha umma kuhusu athari za utumikishwaji wa watoto wadogo, Wananchi wanaweza kuchukua hatua kwa kutoa taarifa kuhusu matukio ya utumikishwaji, kushiriki katika harakati za kutetea haki za watoto, na kusaidia katika kuweka mazingira salama kwa watoto.

Serikali, NGOs wananchi, na mashirika ya kimataifa wanahitaji kufanya kazi pamoja ili kuzidisha jitihada za kupambana na utumikishwaji wa watoto wadogo. Ushirikiano huu unaweza kujumuisha kubadilishana uzoefu, kuendeleza mikakati ya pamoja, na kuimarisha mifumo ya sheria na utekelezaji.

Suluhisho lingine ni kuweka mkazo kwenye elimu na ufahamu kuhusu haki za watoto. Elimu bora na endelevu inaweza kusaidia kubadilisha mitazamo na mila potofu zinazochangia utumikishwaji wa watoto. Pia, ni muhimu kukuza fursa za kiuchumi kwa familia na kujenga mifumo ya ulinzi wa watoto ili kuwalinda na kuwawezesha.

Uhamasishaji kuhusu uelewa na kushiriki katika kampeni za kupinga utumikishwaji, kama vile kampeni za kutetea haki za watoto na kuelimisha jamii, inaweza kuleta mabadiliko makubwa. Umuhimu wa kuwapa sauti watoto wenyewe na kusikiliza maoni yao, kwani wao pia ni sehemu muhimu ya mchakato wa kutafuta suluhisho la tatizo la utumikishwaji katika eneo husika.

Naamini kwamba makala hii itakuwa ni mwanga wa matumaini na mwito wa hatua za haraka katika kukabiliana na utumikishwaji wa watoto wadogo.

Post a Comment

0 Comments