Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

AFYA: VIFO VYA UZAZI NA WATOTO WACHANGA

 

Na, John Kabambala: Sekta ya Afya ni muhimu katika ustawi wa watu, uimarishaji wa nguvu kazi na ukuzaji wa maendeleo ya taifa. Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuboresha utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vipya vya afya, ukarabati wa vituo vilivyopo, utoaji wa vifaa tiba na upatikanaji wa dawa muhimu.

Katika tathmini kuhusu mwenendo wa utoaji huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; ilibainika kuwa, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya, sekta ya afya bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa wataalamu, ufinyu wa bajeti, mazingira duni ya kazi, upungufu wa miundombinu na uhaba wa dawa na vifaa tiba.

Makala hii inaangazia juu ya changamoto zinazoonekana katika sekta ya afya, na inabainisha maeneo muhimu ambayo yanahitaji kusimamiwa kwa umakini na kupendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Serikali na wadau wengine ili kutatua changamoto zilizobainika.

HATUA ZA KUPUNGUZA VIWANGO VYA VIFO VYA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA.

Kwa mujibu wa Mwongozo wa mapitio ya vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga uliotolewa Oktoba 2019 unaeleza kuwa Kifo cha Mama mjamzito ni kifo cha mwanamke kinachotokea wakati akiwa mjamzito au ndani ya siku 42 baada ya mimba kutoka, bila kujali miezi ya ujauzito na eneo la ujauzito kutokana na sababu zinazohusiana au kuchochewa na ujauzito au usimamizi wake, lakini sio kwa sababu za ajali au sababu zisizozuilika. Vifo vya watoto wachanga ni kifo cha mtoto mchanga ndani ya siku 28 za kwanza tangu kuzaliwa.

Aya ya 4.4 ya Mpango wa Taifa wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga wa Mwaka 2021 ‘one plan III’ uliotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeonyesha shabaha ya vifo vya wajawazito kupunguzwa kutoka 250 hadi 100 kwa vizazi hai 100,000. Hata hivyo viwango hivyo vinatofautiana na shabaha ya vifo 180 kwa vizazi hai 100,000 iliyoelezwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021/22-2025/26.

Kulingana na takwimu zilizochapishwa kwenye tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia mwaka 2020, Tanzania ilikuwa na makadirio ya vifo vya wajawazito 238 kati vizazi hai 100,000.

Mpango wa Taifa wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga wa Mwaka 2021 ‘one plan III’ unaeleza shabaha ya kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 20 kwa vizazi  hai 1,000 hadi vifo 15 kwa vizazi 1,000 ifikapo 2025.

Hata hivyo, viwango hivyo vinatofautiana na viwango tarajiwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021/22-2025/26 ambao unaonyesha kuwa Tanzania imepanga kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka vifo 36 hadi 30 katika vizazi 1000 ifikapo mwaka 2025/26.

Katika mwaka 2021/22, ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali ya mwaka 2021/22 ilibainisha kwamba, kulikuwa na ongezeko la viwango vya vifo vya wajawazito zaidi ya lengo la vifo 100 kwa kila vizazi hai 100,000 katika Mamlaka 20 za Serikali za Mitaa.

VIWANGO VYA VIFO HUKADIRIWAJE?

Viwango vya vifo vya wajawazito katika vizazi hai 100,000 hukadiriwa kwa idadi halisi ya vifo vya wajawazito vilivyotokea katika vizazi hai halisi kwenye  Halmashauri husika. Viwango hivyo vinapatikana kwa kuchukua idadi ya vifo halisi kugawanywa na vizazi hai halisi na kuzidishwa na vizazi hai 100,000.

Mfano H/Mji Geita mwaka 2021, kiwango ni (27/12,931*100,000=209) Licha ya kwamba viwango vya vifo vya wajawazito katika Mamlaka 13 za Serikali za Mitaa kuwa chini ya vifo 100 kati ya vizazi hai 100,000, kwa miaka miwili takwimu zilizopatikana zinaonyesha kuwa idadi ya vifo vya wajawazito ilikuwa inaongezeka na kuashiria kuwa katika miaka ijayo viwango hivyo vitakuwa juu ya shabaha inayokusudiwa.

Hata hivyo ripoti hiyo inabainisha katika mwaka 2021/22 niligundua viwango vya vifo vya watoto wachanga katika Mamlaka 2 za Serikali za Mitaa vilikuwa ni vifo 135 na vifo 49 kwa watoto 1000 waliozaliwa ambavyo viwango vikubwa zaidi kuliko lengo la vifo 30 kwa watoto 1000 wanaozaliwa kama ilivyoelezwa katika Mpango wa ‘One Plan III’.

Vifo vya watoto wachanga 6335 katika Mamlaka 20 za Serikali za Mitaa kwa miaka miwili; hata hivyo, kiwango cha vifo kwa watoto 1000 wanaozaliwa hakikuweza kupatikana baada ya kukosekana taarifa za idadi ya watoto waliozaliwa. Idadi ya vifo vilivyotokea ni kubwa inayolazimu kuchukuliwa hatua ili kuondoa vifo vya watoto wachanga na kufikia shabaha ya vifo 30 kwa watoto 1000 wanaozaliwa.

SABABU ZINAZO SABABISHA VIFO VYA UZAZI:

Sababu kuu za vifo vya uzazi ni kuvuja damu wakati wa kujifungua ambayo husababisha zaidi ya robo moja ya vifo, matatizo ya shinikizo la damu wakati wa ujauzito, upungufu wa damu wakati wa ujauzito, kifafa cha mimba na magonjwa yanayohusiana na ujauzito.

Sababu nyingine ni kuchelewa kwa wajawazito katika vituo vya afya ili kupata huduma ya matibabu kwa wakati wa uchungu, watoa huduma za afya ya msingi na wakunga kutokuwa na ujuzi wa kutosha wakati wa kutoa huduma za kujifungua na uhaba wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

SABABU IPI INASABABISHA VIFO VYA WATOTO WACHANGA:

Kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga wa 2021 ‘one plan III’ kukosa hewa kwa watoto wanaozaliwa ni chanzo kikuu cha vifo vya watoto wachanga, ikifuatiwa na kuzaliwa kabla ya wakati na maambuzi ya bakteria.

Vifo hivi vinaweza kuzuilika kwa kuboresha; upatikanaji wa watoa huduma wenye ujuzi, ubora wa huduma kwa wajawazito kabla na baada ya kujifungua na matunzo ya watoto wachanga wanaozaliwa na wanaoumwa. Aidha hatua thabiti zenye ubunifu na ubora zinahitajika kuchukuliwa ili kuzuia viwango vya vifo vya wajawazito na watoto wachanga kufikia shabaha inayolengwa ifikapo mwaka 2025/26.

MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI AMEPENDEKEZA KUWA:

Menejimenti za Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe kuwa huduma bora za afya zinatolewa katika vituo vya afya, kuwapatia wahudumu wa afya ya msingi maarifa na ujuzi wa kutosha ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Kuongeza ufahamu juu ya umuhimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki mapema na kujifungua katika vituo vya afya. Pia, ninashauri Menejimenti za Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa fedha zinazohusu shughuli za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto zinatolewa kama ilivyopangwa ili kuondoa/kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga kama ilivyolengwa”.

 

Post a Comment

0 Comments