Na, John Kabambala:
Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja nchini Tanzania ni kama hadithi ya matumaini vile, inayo lenga kuokoa maisha ya jamii ya watanzania. Ni hadithi inayojumuisha juhudi za serikali na wadau wa afya kuleta mabadiliko chanya katika afya ya jamii ya kitanzania.
Tanzania ni nchi ya Afrika Mashariki katika Ukanda wa Maziwa Makuu, inayojumuisha jumla ya eneo la maji na nchi kavu lenye kilometa za mraba 947,303, ambapo kilometa za mraba 886,040 zinajumuisha ardhi na kilometa za mraba 62,050 zinajumuisha maji (Lake , 2013).
Umewahi kusikia neno,“AFYA MOJA”Unadhani nikitu gani?
Yamkini umewahi kushiriki kuandaa mpango huu, kusoma maeneo mbali
mbali au hata kuusikia ukizungumziwa na wataalamu na viongozi katika ngazi
mbalimbali. Na baadae hukujua kilicho endelea namna ulivyo kamilika na kuanza kufanya
kazi au hukujua kabisa neno hili linahusu kitugani !!!!!.
Mwingiliano miongoni mwa binadamu, wanyama, na mazingira unaendelea kubadilika siku hadi siku, na waliohatarini zaidi ni watoto wachanga, vijana Mama wajawazito na hata Wazee wenye umri mkubwa zaidi. Hali ya ongezeko la idadi ya watu na wanyama, mabadiliko ya tabianchi, matumizi ya ardhi na kuongezeka kwa safari na biashara za kimataifa hutoa fursa za kuenea kwa magonjwa kwa haraka zaidi.
Takriban asilimia 75 ya magonjwa ya kuambukiza yaliyojitokeza hivi karibuni na kuathiri wanadamu kiasili ni magonjwa ya wanyama; aidha, asilimia 60 ya vimelea vya magonjwa yote ya binadamu hivi sasa inatokana na magonjwa yanayopatikana kwa mifugo. Hivyo basi kutokana na hali hiyo hupelekea wanadamu hasa watoto wenye kinga ambazo hazijawa imara zaidi kuwa hatarini kuambukizwa na kuugua na kupata ulemavu na wakati mwingine kufariki.
HISTORIA YA
DHANA YA AFYA MOJA:
Afya Moja inajumuisha taaluma za afya, lakini pia inajumuisha
wataalamu mbalimbali kwa mfano wataalamu wa wanyamapori, wanaanthropolojia,
wachumi, wanamazingira, wanasayansi wa tabianchi na wanasosholojia.
Dhana ya Afya Moja ilitanguliwa na dhana ya 'Dawa Moja' ambayo ina mizizi ya Kiafrika tangu miaka ya 1960, mtaalamu wa epidemiolojia wa Kimarekani Calvin Schwabe, akiwa anafanya kazi yake na wafugaji wa Dinka nchini Sudan alianzisha neno 'Dawa Moja' kutokana na kufanana kwa dawa ya binadamu na ile ya mifugo.
Katika miaka ya 1980, dhana ya 'Dawa Moja' ilibadilishwa na kupanuliwa kuwa 'Afya Moja' ili kuakisi dhana ya afya kwa mfumo mzima wa ikolojia kama ilivyoanzishwa na mashirika ya kimataifa: Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO).
BARA LA AFRIKA MBINU YA AFYA MOJA ILIANZA KUTUMIKA LINI?
Barani Afrika, mbinu ya Afya Moja ilianza kutumika mwaka wa 2018 wakati programu ya Afya Moja ilipokubalika na Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC). Programu hii imezingatia masuala mtambuko ya afya ya jamii ikiwa ni pamoja na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawana magonjwa ya zuonotiki kama maeneo ya kipaumbele.
Kwa mujibu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) inasema Programu ya Afya Moja inajumuisha kikundi kazi cha wataalamu wa Afya Moja (OH-TWG) chenye mgawanyiko ulio na uwakilishi kutoka vitengo vitano vya kitaalamu ambavyo ni: ufuatiliaji na intelijensia ya magonjwa, maandalizi ya dharura na kukabiliana na maafa,mifumo ya maabara, taasisi za afya ya jamii,utafiti, udhibiti na uzuiaji wa magonjwa.
Wakati wa Mkutano wa 35 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki uliofanyika mwaka 2017, iliamuliwa kwamba dhana ya Afya Moja itumiwe na mataifa hayo na Jukwaa la Afya Moja la Jumuiya ya Afrika Mashariki lianzishwe na kuwezeshwa kufanya kazi.
Mnamo mwaka wa 2019, Baraza la 19 la Kisekta la Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki liliagiza Sekretarieti ya Jumuiya hiyo kuimarisha ushirikiano na uratibu wa sekta mbalimbali kwa kuanzisha Mkakati wa Afya Moja wa kikanda. Inatarajiwa kwamba kupitishwa kwa mkakati huu kutatoa mwongozo wa utayari wa fani na sekta mbalimbali katika kujiandaa, kuzuia, kutambua na kukabiliana na matishio ya afya ya jamii katika mipaka ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na hatimaye kuboresha uratibu katika kukabiliana, kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza yanayohusiana na Afya Moja kwa wanadamu, wanyama na mazingira.
MPANGO WA AFYA MOJA TANZANIA UMEUNGWA MKONO LINI?
Nchini Tanzania, dhana ya Afya Moja, imeungwa mkono na sekta mbalimbali, na ilikubaliwa kwa mara ya kwanza katika udhibiti wa mlipuko wa Homa ya Bonde la Ufa mwaka 2007. Katika kipindi hicho, idadi ya mitandao na majukwaa ya Afya Moja yaliundwa.
Haya ni pamoja na Kituo cha Kusini mwa Afrika cha kufuatilia Magonjwa ya Kuambukiza (SACIDS), Mtandao wa Afya Moja wa Afrika ya Kati na Mashariki (OHCEA), Muungano wa Utafiti wa Kiafrika wa Mfumo wa Mazingira na Afya ya Idadi ya Watu (AfriqueOne) na Mitandao ya Kitaifa ya Afya Moja ya Utafiti iliyoimarishwa ya Magonjwa ya Kuambukiza (NRN-Biomed), Kikosi Kazi cha usistisekosi (Cysticercosis) katika Afrika Mashariki na Kusini (CWGESA) na Afya kwa Wanyama na Maisha (HALI).
Mitandao hii na majukwaa mengi yalianzishwa kwa ushirikiano na wanasayansi wa utafiti katika vyuo vikuu na taasisi za utafiti ili kukuza utafiti wa Afya Moja na kutoa uthibitisho kwa watunga sera. Ajenda ya Kitaifa ya Afya Moja nchini Tanzania ilibuniwa na kurasimishwa wakati wa Mkutano wa Pili wa Wanasayansi wa Afya Moja pamoja na Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR) uliofanyika mwaka 2013.
Milipuko ya magonjwa ambayo hupunguza upatikanaji wa wanyama hai na mazao ya mifugo inaweza kupunguza mapato ya kaya, kudhoofisha mlo wa wanakaya, kudhoofisha hali ya lishe na kuongeza hatari kwa afya, hasa kwa wanawake na watoto.
Hata hivyo, milipuko inaweza kudhoofisha upatikanaji wa soko kwa bidhaa hizo. Ukosefu wa usalama wa chakula kwa muda mrefu pia husababisha tabia hatarishi zinazohusiana na upatikanaji wa nyama, mfano hakuna mtu ambaye ana uhakika wa usalama wa chakula angefikiria kula mzoga. Madhara ya magonjwa ya wanyama yanaenea kwa wafanyakazi wanaofanya kazi za uzalishaji na uchakataji – kwa maao ya mifugo, kilimo, wasafirishaji, na wauzaji. Hivyo nimuhimu kuzingatia mwingiliano kati ya wanyama na makaazi ya binadamu, ili kuepusha ongezeko la mlipuko ya magonjwa.
0 Comments