Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

ELIMU NA KUKABILIANA NA MIMBA ZA UTOTONI KWA WASICHANA TANZANIA.

 

Picha kutoka un news.

Na, John Kabambala: 

Mimba za utotoni ni suala la kijamii na afya linaloathiri wasichana duniani kote, ikiwa ni pamoja na Tanzania. Mimba za utotoni ni suala linalosababisha wasichana kukatisha masomo yao na kuathiri maendeleo yao ya kielimu na kijamii. Katika juhudi za kukabiliana na tatizo hili, Serikali ya Tanzania imechukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuruhusu wasichana walio pata mimba na kujifungua kuendelea na masomo yao. Hapa tutachunguza suala la mimba za utotoni na uamuzi wa serikali kuhusu kuruhusu wasichana hawa kuwarejesha shuleni kuendelea na masomo.

MIMBA ZA UTOTONI TANZANIA:

Mimba za utotoni ni tatizo kubwa nchini Tanzania, na lina athari kubwa kwa maendeleo ya wasichana. Sababu za mimba za utotoni ni pamoja na ukosefu wa elimu ya Afya ya uzazi, umasikini, ndoa za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia, na upatikanaji mdogo wa huduma za afya ya uzazi. Kulingana na Taarifa ya Hali ya Watoto Duniani ya mwaka 2021, asilimia 27% ya wasichana nchini Tanzania wanapata mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Mimba za utotoni zinaweka vikwazo vikubwa katika maendeleo ya wasichana. Wasichana wengi wanaopata mimba wanakatishwa masomo yao, na mara nyingi wanakumbana na unyanyapaa na ubaguzi wa kijamii. Hii inaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa wasichana hawa, ikiwa ni pamoja na kupoteza fursa za kielimu na kiuchumi.

UAMUZI WA SERIKALI WA KURUHUSU WASICHANA WALIO PATA MIMBA KUENDELEA NA MASOMO:

Mwishoni mwa mwaka 2021, Serikali ya Tanzania ilichukua hatua za kurekebisha hali hii na kutoa fursa zaidi kwa wasichana walio pata mimba kuendelea na masomo. Hata hivyo ikimbukwe kwamba mwaka 2017, Serikali ilipitisha sera mpya inayoruhusu wasichana walio pata mimba kurudi shuleni baada ya kujifungua. Uamuzi huu ulifanywa kwa lengo la kuhakikisha kwamba wasichana hao hawakatishwi masomo yao na wanapata nafasi ya kuendelea na elimu yao.

Hatua hii ilionesha maana kubwa katika kuboresha hali ya wasichana walio pata mimba. Nakuwapa fursa ya kuendelea na masomo yao na kujenga mustakabali bora zaidi kwa maisha yao. Hata hivyo, kuna changamoto katika utekelezaji wa sera hii, kama vile ubaguzi wa kijamii na unyanyapaa dhidi ya wasichana walio pata mimba.

Kufuatia waraka huo wa Serikali ulioelekeza wanafunzi wa kike waliopata ujauzito warejee shule katika mfumo rasmi baada ya kujifungua wadau wa Elimu nchini waliipongeza Serikali kwa hatua hiyo. Lakini nikwa namna gani mwendelezo wa program hii unaendelea na kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Herriet Mkaanga

Herriet Mkaanga, mwanaharakati wa watoto wa kike na Mkurugenzi wa Shirika la My Health Foundation  ambalo limekua likipigania suala hili kwa muda mrefu, aliishukuru  Serikali kwa hatua hiyo na kutoa maoni yake kuwa wapatiwe Elimu ya saikolojia kabla ya kurejeshwa Shule ili wakafanye vizuri zaidi.

Mkaanga pia wakati wa mahojiano yangu alisema juhudi nyingine zinazotakiwa kuchukuliwa dhidi yao ni kuwezesha mazingira yao ya kujifunzia ili wasiingie tena katika ushawishi wa kupata ujauzito ikiwemo, kuwasaidia taulo za kike, vyakula kwa Shule zenye mabweni.

kwa mujibu wa Takwimu za Elimu ripoti ya Best 2020 ilieleza jumla ya idadi ya wanafunzi wa kike 1,135 sawa na 0.7% walipata ujauzito katika Shule za Msingi, ilhali shule za Sekondari walikua 5,398 sawa 5.5% mwaka 2019.

Aidha matukio ya Mimba za utotoni yaliyoripotiwa Ofisi ya Afisa ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, yaliongezeka kutoka 800 mwaka 2019/2020 hadi kufikia zaidi ya 1200 Mwaka 2020/2021.

Akithibitisha Takwimu hizo Afisa usatawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro Bi, Jessica Kagunila, alisema sababu ya Mimba za utotoni kuongezeka inachangiwa na Mila na Desturi za Mkoa huo pamoja na malezi yasiyo mazuri ya watoto.

“Tukianza kwa Mwaka 2019/2020 matukio ya mimba za utotoni yaliyoripotiwa ni 800 lakini tukija kwa Mwaka 2020/2021 yameongezeka hadi kufikia zaidi ya 120, hii ni kutokana na Mila na desturi na malezi yasiyo mazuri kwa upande wa walezi na wazazi’’ alisema Jessica Kagunila

Kwa mujibu wa Ofisi ya muendesha Mashtaka Mkoa wa Morogoro DPP, matukio ya mimba za utotoni ambayo kisheria huitwa matukio ya ubakaji yanaongezeka kutokana na watuhumiwa wa makossa hayo kutoa Rushwa kwa waathirika na kesi kukosa ushahidi Mahakamani, alisema kaimu uendesha mashtaka wa Mkoa wa Morogoro Flora Massawe.

“Inatokea mara nyingi mahakamani, mashahidi wengi ambao ni wahanga watoto wanakuja kugeuka yaani ule ushahidi waliotoa Polisi kwamba wamefanyiwa kitendoi cha ubakaji na flani wakifika mahakamani wanakuja kukataa, na hii tumebaini kutokana na wazazi kuridhia kufanya makubaliano na mtuhumiwa kuna kiasi cha Pesa wanalipana, basi huku kesi zinaharibika’’ alisema Flora Massawe

Jessica Kagunila

Afisa ustawi wa Mkoa wa Morogoro Bi, Jessica Kagunila alieleza namna ambavyo watazidi kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha matukio ya Mimba na Ndoa za utotoni yanapungua.

Bi, Jessica alisema “Elimu sio suala la ustawi wa Jamii peke yake, maendeleo ya Jamii na wadau wengine wa Elimu tutaendelea kushirikiana kuzunguka shuleni kutoa elimu na hata kuwafikia wazazi kadri tutakavyoweza pamoja na walimu ambao wanakaa muda mrefu na watoto’’

Katika kumulikia juhudi za Sekta binafsi kushirikiana na Serikali juu ya kutokomeza Mimba za utotoni Mkoa wa Morogoro, Tanzania kids time ilizungumza na Mratibu wa Miradi Evarist Momburi, kutoka Shirika la SAWA WANAWAKE TAZNANIA lililojikita katika kusimamia ulizi wa Mtoto na utoaji Elimu jumuishi kwa Shule za Msingi, ili kusikia maoni yake pamoja na juhudi zao katika hili.

“kama tunataka tupunguze hili tatizo la Mimba za utotoni, dawa yake ni kujenga mabweni na kujenga Shule shikizi ambazo zitasaidia kupunguza ule umbali wa mwanafunzi kutembea kuifata Shule ilipo, na hili tulifanya utafiti tukagundua watoto wengi walikuwa wanakatiza masomo kwa sababu walikua wanapata changamoto ya umbali kuifata Shule ilipo’’ Alisema Evarist Momburi.

Alisema katika Mkoa wa Morogoro Shirika la, SAWA WANAWAKE TANZANIA tayari limeshaboresha mabweni ya wasichana katika Shule za Sekondari za DOMA na MVOMERO na Mwaka 2022 wamejipanga kuifikia Shule ya Sekondari WAMI DAKAWA kupitia Mradi wake wa TUWALINDE WATOTO.

Penina Sangiwa

Kwa upande wake Bi, Penina Sangiwa Afisa Elimu kutoka Shirika la umoja wa kimataifa la kuhudumia watoto, alisema Serikali imepiga hatuka kubwa ya kuhakikisha kiloa mtoto mwenye umri wa kusoma anapata Elimu, lakini bado kunajitihada zinahitajika kuhakikisha lengo hilo linatimia.

Penina aliongeza kuwa ni jitihada kubwa zinatakiwa kuchukuliwa na Serikali, wadau wa Elimu na mashirika na Taasisi mbalimbali kueneza Elimu ya Afya ya uzazi kwa wasichana Shuleni ili kuepukana na mimba ambazo zinaweza kujitokeza tena.

Post a Comment

0 Comments