Advertisement

Responsive Advertisement

Navigation Menu

MWANAMKE SHUJAA WA KILIMO HIFADHI KUTOKA KIGOMA TANZANIA:FAO

Hadija Alisido akipokea zawadi ya zana za kilimo kutoka kwa mgeni rasmi na muakilishi mkaazi wa umoja wa mataifa nchini Tanzania.

Na, John Kabambala.

Mwanamke mmoja jasiri, mwenye macho yenye ndoto na mikono iliyoshiba ardhi, alijulikana kwa jina la Hadija Alisido  mama wa familia na mkulima wa kawaida katika kijiji chake. Kilimo kilikuwa chanzo cha kipato chake na cha familia yake, lakini matatizo yalikuwa hayakwisha kumwandama. Hali ya hewa ya kutatanisha, udongo usiokuwa na rutuba, na mavuno duni yalikuwa vitisho vikubwa kwa kipato chake.

Lakini kama ilivyotokea katika visa vingine vingi vya mafanikio, Hadija  alipata fursa ya kipekee ambayo ilibadilisha kabisa mustakabali wake. Fursa hiyo ilikuwa mafunzo ya kilimo hifadhi kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kupitia mradi wa Pamoja Kigoma (KJP) unaotekelezwa mkoani humo kwa ufadhili wa mashirika ya umoja wa mataifa. Mafunzo haya yalimpa Hadija mbinu mpya za kilimo, zilizokuwa zikitumia ardhi kwa ufanisi, kulinda mazingira, na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Jinsi Hadija  alivyosikiliza kila somo kwa makini na kujifunza kila hatua ya kilimo hifadhi kwa vitendo, ndivyo ndoto yake ya kuleta mabadiliko kijijini ilivyokua na kuwa kubwa.Kisa  hiki kinaendelea kusimulia safari ya Hadija  kutoka kwenye udongo usiokuwa na matumaini hadi kwenye mavuno mengi, kutoka kwenye ukame wa kutisha, na kutoka kwe kijiji kidogo kilichokuwa hakina matumaini hadi kuwa kielelezo cha mafanikio na matumaini kwa wanawake wa vijijini nchini Tanzania.

Mwanzoni Hadija alikuwa akilima eneo la ukubwa wa heka tano na kila heka moja kwa wastani alikuwa akipata mavuno ya gunia kumi, ambapo kwa heka zote tano jumla alikuwa akipata gunia hamsini zisizo pungua kwa msimu mmoja, kiwango hicho cha mavuno aliokuwa akiyapata Hadija hayakuwa yanakidhi mahitaji yake kwa mujibu wa malengo yake ya kila mwaka.

Miongoni mwa malengo yake makubwa ya kila mwaka yalikua ni kuishi masha mazuri, kuwasomesha watoto wake kwenye shule zenye gharama kubwa kwa ajili ya kupata elimu ya uhakika, kujenga nyumba nzuri yenye mahitaji yote ya msingi laniki pia na kuongeza shughuli zake za kilimo. Vuta nikuvute malengo hayo hayakuwa yanatimia siku hadi siku na mwaka hadi mwaka kwa masikitiko makubwa.

TATIZO LA KILIMO KATIKA KIJIJI CHAKE. 

Tatizo kubwa ilikuwa ni changamoto za Ukame na Upungufu wa Maji, Ukame mara kwa mara uliathiri kwa kiasi kikubwa mavuno ya mazao. Maji ya mvua yalikuwa yanapungua, na udongo uliathirika kutokana na upungufu wa uhifadhi wa maji. Aidha familia nyingi zilikuwa zinapambana na umaskini kutokana na mavuno duni ya mazao, ambayo yalitokana na mazingira ya udongo na hali mbaya ya hewa. Kutegemea Mazao ya Kilimo cha kawaida kisicho kuwa na maarifa ya kutosha, Wakulima wengi walipata mazao machache kila msimu kama mahindi, viazi, mihogo na maharage na hawakutumia mbinu bora za kilimo ambazo zingesaidia kuongeza uzalishaji. Hii ilisababishwa na ukosefu wa elimu ya kilimo kinacho himili mabadiliko ya hali ya hewa.

CHANZO CHA TATIZO

Chanzo kikuu cha matatizo haya kilikuwa ukosefu wa maarifa na mbinu za kilimo bora katika kijiji hiki. Wanakijiji walikuwa wakifuata kilimo cha mazoea kilimo ambacho wazee wao walikitumia tangu enzi na ezni ambapo hakikuwa na ufanisi tena wa kutosha kuwa na uzalishaji wa mavuno mengi kwa kipindi hiki na kujibu changamoto za mazingira na mahitaji ya wakulima.


SULUHISHO LA MAFANIKIO YA HADIJA.

Suluhisho la mafanikio ya Hadija lilikuwa maarifa na mafunzo ya kilimo hifadhi kutoka FAO. Mafunzo haya yalimpa ujuzi na mbinu mpya za kilimo ambazo zilikuwa na manufaa makubwa katika kupambana na changamoto za kilimo zilizokuwa zinamkabili. Mbinu za Kilimo Hifadhi: Hadija alijifunza kwa undani mbinu za kilimo hifadhi, kama vile kupanda mazao kwenye mistari na matumizi ya mbolea za asili. Hizi zilikuwa njia zinazosaidia kuhifadhi ardhi na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Uhifadhi wa Maji: Mafunzo yalimpa Hadija maarifa ya kuhifadhi maji, na hivyo kudhibiti upatikanaji wa maji wakati wa ukame. Hii ilisaidia kulinda mazao na kuwa na uhakika wa chakula hata wakati wa hali mbaya ya hewa. Kilimo cha Mzunguko wa Mazao: Hadija alipata ujuzi wa namna kulima kilimo cha mzunguko wa mazao ambacho kiliboresha uzalishaji wa ardhi yake na kumuepusha na kuvu.

Kupitia mbinu za kilimo hifadhi, Hadija alifanikiwa kuongeza mavuno ya mazao yake mwaka huu alilima eneo la ukubwa wa heka mbili na kuvuna mazao kiasi cha gunia miamoja na ishirini za mahindi (120) kwa maana kila heka moja alipata gunia sitini sitini (60).Mavuno haya yalikuwa ya kustajabisha maana hakuwahi kutokea katika maisha yake yote ya kilimo kupata mazao kiasi hicho.

Hata hivyo  kilimo hifadhi kilisaidia kupunguza athari za ukame kwa kutumia mbinu za uhifadhi wa maji, na kuboresha hali ya udongo. Hadija hakuishia hapo tu, alilima mihogo na mavuno yake kwa mwaka huu amepata tani sita ambazo alipouza mihogo hiyo alipata kiasi cha Tshs, 7,820,000/= kiasi ambacho alikuwa akikisikia tu kwa watu wengine kikitajwa lakini sasa amekipata mwenyewe kwa kuuza mihogo alio ilima kwenye shamba lake mwenyewe kwa kufuata elimu ya kilimo hifadhi iliotolewa na FAO.

Ndoto yake ya kujenga nyumba na kusomesha watoto wake kwenye shule zenye uhakika wa elimu imetiamia, ameweza kuwalipia watoto wake ada katika shule hizo na kuboresha maisha yake ya nyumbani, kupitia yeye jamii yake imeona sasa kumbe kilimo hifadhi ni mkombozi na niuhakika wa kupata mavuno mengi yakutosha.

USHAURI WA NEEMA KWA WANAWAKE WA KIJIJINI NA JAMII KWA UJUMLA

Hadija anatambua kuwa maarifa na mafunzo ya kilimo hifadhi yalimwezesha kuleta mabadiliko katika maisha yake na kijiji chake anaona nivema sasa kutoa ushauri wake kwa wanawake wa kijijini na jamii kwa ujumla:

Jifunzeni na Kuweka Muda wa Kujifunza: Hadija anaamini kuwa maarifa ni nguvu. Anawahimiza wanawake wa kijijini kujifunza mbinu mpya za kilimo na kujitolea kwa mafunzo. Kuweka muda wa kujifunza kunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika uzalishaji wa mazao.

Shirikianeni na Jifunzeni Kutoka Kwa Wenzenu: Hadija anasisitiza umuhimu wa kushirikiana na kujifunza kutoka kwa wenzao. Kuanzisha vikundi vya wakulima wa kijijini kunaweza kuwa njia nzuri ya kusambaza maarifa na mbinu bora za kilimo.

Tumia Ardhi kwa Ufanisi: Hadija anaonyesha umuhimu wa kuhifadhi ardhi na kuilinda. Kwa kutumia mbinu za kilimo hifadhi, ardhi inaweza kuwa na uzalishaji wa muda mrefu na kuwa na rutuba zaidi.

Jifunzeni Kuendesha Miradi ya Maji: Hadija  anahimiza jamii, utunzaji wa rasilimali muhimu ya maji, na kudhibiti upatikanaji wa maji kunaweza kuwa na athari kubwa katika kilimo na maisha ya kijijini.

Kuwa Mfano kwa Wenzako: Hadija anawaambia wanawake wa kijijini kuwa wanaweza kuwa mifano kwa wenzao. Kwa kufuata mafanikio yao na kushirikisha maarifa yao, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii zao. Kusaidiana na Kusimamia Rasilimali: Jamii inapaswa kusaidiana na kusimamia rasilimali kwa uwajibikaji. Kwa kushirikiana, wanaweza kuboresha hali ya maisha ya kijijini kwa ujumla kwani wanawake wa vijijini ni mashujaa wa chakula.

Kupitia siku ya wanawake wa vijijini FAO imemzawadia vifaa muhimu vya kilimo mbele ya muwakilishi mkaazi wa Umoja wa Mataifa Zlantan Milisic katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma. Nasasa Hadija anasema “natoa shukrani na pendo lisilo kifani kwa shirika la chakula na kilimo la umoja wa Mataifa (FAO) kwa maarifa na elimu ya kilimo hifadhi familia yangu inaneemeka kwa mavuno haya, msimu ujao nimejipanga zaidi kuliko uliopita”

Kwa ushauri wa Hadija, wanawake wa kijijini wanaweza kuwa nguvu kubwa katika kuleta mabadiliko katika kilimo na jamii zao. Kupitia kujifunza, kushirikiana, na kushirikisha maarifa, wanaweza kuwa chachu ya maendeleo na kuondoa umaskini katika vijiji vyao. Kisa cha kweli cha Hadija ni kielelezo cha mafanikio na matumaini makubwa, na ushauri wake unaweza kuwa mwongozo wa kuleta mabadiliko katika vijiji vya Tanzania na kote duniani.

Post a Comment

0 Comments